Jumapili 9 Novemba 2025 - 10:37
Taifa lililodhulumiwa la Sudan leo linangojea uungaji mkono wa pamoja wa Umma wa Kiislamu

Hawza/ Hujjatul-Islam Sadiq Jafari, akielezea wasiwasi mkubwa kuhusu kuendelea kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe na mgogoro wa kibinadamu nchini Sudan, ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za haraka za kusitisha mapigano na kuiunga mkono jamii ya watu wanyonge wa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam Sadiq Jafari, mjumbe mwandamizi wa Baraza la Umoja wa Waislamu wa Pakistan, akionesha wasiwasi mkubwa juu ya kuendelea kwa vita vya ndani na mgogoro wa kibinadamu nchini Sudan, amesisitiza umuhimu wa hatua za dharura za kimataifa kusimamisha mapigano na kusaidia wananchi wanaoteseka.

Katika mwendelezo wa hotuba yake, akibainisha kuwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, mapigano ya damu yameendelea katika miji mbalimbali ya Sudan, hasa Darfur na Al-Fashir, alisema: “Vita hivi vya umwagaji damu vimeisukuma nchi hadi ukingoni mwa maangamizi. Maelfu ya raia, wakiwemo wanawake na watoto, wameuawa au kulazimika kuyakimbia makazi yao. Mamilioni ya watu wanalazimika kuishi katika kambi bila maji, chakula, au huduma za afya, huku hospitali, nyumba za ibada, na maeneo ya makazi yakilengwa na mashambulizi. Hali hii ni uvunjaji wa wazi wa haki za binadamu, sheria za kimataifa, na thamani za kibinadamu na Kiislamu, na inahitaji kushughulikiwa mara moja.”

Mtaalamu huyo wa kidini kutoka Pakistan, akirejelea wajibu wa taasisi za kimataifa kuhusu mgogoro wa Sudan, alisema: “Baraza la Umoja wa Waislamu wa Pakistan linazihimiza taasisi za kimataifa, hususan Umoja wa Mataifa, Shirika la Ushirikiano wa Kiislamu, Umoja wa Afrika na mashirika ya kutetea haki za binadamu, kuchukua hatua za haraka na zenye ufanisi za kuishinikiza pande zinazopigana kusitisha mapigano na kurahisisha njia za misaada ya kibinadamu kufikishwa kwa waathirika.”

Akiendelea kwa kusisitiza haja ya kushughulikia uhalifu uliofanywa, aliongeza: “Uchunguzi wa wazi na usiopendelea upande wowote kuhusu mauaji ya halaiki ya raia na uhalifu wa kivita unapaswa kufanyika, na vikosi vya kulinda amani chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa vipelekwe katika maeneo yenye machafuko ili kuhakikisha usalama wa raia. Dhamiri ya dunia inapaswa kuamka, na jumuiya ya kimataifa inatakiwa kusimama pamoja na watu waliodhulumiwa wa Sudan, si kubaki watazamaji wa mateso na maangamizi yao.”

Mwanachuoni huyo wa Kiislamu wa Pakistan alihitimisha kwa kusisitiza: “Kupambana na dhulma na uvamizi katika sehemu yoyote ya dunia ni sehemu ya imani na ni jukumu la kidini. Watu wanyonge wa Sudan leo wanahitaji zaidi kuliko wakati mwingine wowote msaada wa Umma wa Kiislamu. Tuko pamoja nao kwa sauti na kwa vitendo, na tunasisitiza juu ya kuendeleza misaada ya kibinadamu na juhudi za kutekeleza haki. Tuna yakini kuwa siku itafika ambapo nguzo za dhulma zitaporomoka, na alfajiri ya uadilifu na ukweli itachomoza.”

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha